Scroll to top

CEO Roundtable yashauri vijana wainuliwe katika Uongozi kuelekea Uchumi wa kati wa Viwanda

MKUTANO wa wajumbe wa CEO Roundtable umeshauri kuwepo kwa msukumo wa kuwawezesha vijana katika nafasi za uongozi wa taasisi mbalimbali ili kutengeneza fursa zitakazowapa uwezo vijana hao kusimama imara katika nafasi za uongozi.

Rai hiyo imetolewa Jijini Dar es Salaam juzi na Mkurugenzi wa Kanda wa Kampuni ya Jubilee Julius Kipng’tich wakati wa mkutano wa wakuu hao uliolenga kutathimini hali mabadiliko ya kimfumo katika soko na mikakati yao kuendana na sera na miongozo mbalimbali ya Serikali.

Katika mkutano huo ulioudhuriwa na wakurugenzi kutoka taasisi mbalimbali, Kipng’tich alisema kuna haja ya vijana hao ambao ndiyo viongozi wajao, kujengewa uwezo huo utakaowasaidia kushika nafasi hizo na hivyo kuleta mabadiliko chanya katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali watakayopewa.

“Jamii inapaswa kuchukua hatua katika kuwasaidia vijana kuleta mabadiliko, Afrika ina fursa nyingi na uwezo wa kufanya mambo mazuri ambayo kama zitaweza kufanyiwa kazi zitasaidia maendeleo kukua huku tukiamini kuwa vijana wana nafasi ya kutufikisha hapo” alisema Kipng’tich.

Aidha alisema katika kufikia malengo hayo, vijana wanapaswa kujiwekea malengo katika kutimiza ndoto zao za kuwa viongozi huku wakiiga mfano wa mambo mazuri yanayofanywa na viongozi waliopo sasa hatua aliyosema kuwa itawasaidia katika mipango yao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa maofisa watendaji wakuu wa kampuni (CEOrt) Sunil Mittal, alisema pamoja na hatua mbalimbali ambazo bara la Afrika linapitia, teknolojia inapaswa kutumiwa vizuri ili kuongeza kasi ya maendeleo hayo.

Pamoja na hayo pia alisema uwepo wa sera mbalimbali zinazosaidia kuleta mabadiliko ni vizuri zikasimamiwa ipasavyo ili kuwawezesha vijana kupiga hatua ambazo pamoja na mambo mengine ndiyo chachu ya maendeleo ya nchi na Afrika kwa ujumla.

CEO Roundtable ni jukwaa la majadiliano ya sera ambalo huwakutanisha Maafisa watendaji wakuu zaidi ya 150 wa kampuni zinazoongoza nchini Tanzania.

Source: http://francisdande.blogspot.com/2019/11/ceo-roundtable-yashauri-vijana.html